News
Ziara ya Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Masjala ya Ardhi ya Kijiji cha Melela-Mvomero DC
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezindua jengo la masjala ya ardhi kijiji cha Melela wilayani Mvomero, lililojengwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) na kumuelekeza Mtendaji wa Kijiji kuhakikisha linatumika ipasavyo kuwahudumia wananchi wa kijiji hicho.
Mhe. Jenista ameridhishwa na ubora wa jengo la ofisi hiyo ya masjala ya ardhi, ambalo amesisitiza litumike kupima mashamba ya wananchi na kutoa hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa Kijiji cha Melela ili wazitumie kuomba mikopo katika taasisi za kifedha ambayo itawawezesha kujishughulisha na kilimo na ujasiliamali.
“Serikali inataka ofisi hii iwe ni sehemu muhimu itakayowawezesha wananchi wa Melela kupata maendeleo, wataalam wote waitumie ofisi hii kuwahudumia wananchi pindi wanapofuata huduma, kama ambavyo Serikali imekusudia,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Ameongeza kuwa, uwepo wa ofisi hiyo umeondoa tatizo la uhaba wa ofisi, hivyo kuondoa kisingizio cha baadhi ya watumishi wa Kijiji cha Melela kutowajibika ipasavyo kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa Benki ya CRDB, Bw. Emmanuel Meela ameipongeza Serikali kupitia MKURABITA kwa kujenga ofisi ya Masjala ya Ardhi ambayo itawasaidia wananchi kurasimisha ardhi na kupata hati miliki za kimila ambazo zitawawezesha kukopa katika taasisi za kifedha kwa lengo kufanya shughuli za maendeleo.
Naye, Meneja wa Benki ya NMB Mvomero, Bw. Innocent Kato amewathibitishia wananchi wa Kijiji cha Melela kuwa Benki ya NMB inazitambua Hati za Hakimiliki za Kimila, na kuongeza kuwa mpaka hivi sasa benki hiyo imepokea dhamana ya takribani ya kiasi cha shilingi milioni 600 hadi 700 zilizowekwa na wananchi wenye uhitaji wa kuendesha shughuli za kiuchumi wilayani Mvomero.
Akizungumzia utayari wa taasisi za kifedha kutoa mikopo kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amewaasa wananchi wa Kijiji cha Melela kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo.