Tanzania emblem

The United Republic of Tanzania

Property and Business Formalization Program

News

MKUU WA WILAYA YA DODOMA MHE. JABIR SHEKIMWERI AFUNGUA KIKAO CHA WADAU WA URASIMISHAJI NA UENDELEZAJI WA BIASHARA ZA MACHINGA KATIKA JIJI LA DODOMA


Katika hotuba yake ya uzinduzi wa kikao cha Wadau wa Urasimishaji na uendelezaji wa biashara za Machinga katika Jiji la Dodoma, Mhe. Mkuu wa Wilaya aliwaeleza Washiriki kuwa Serikali imetoa maagizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ya kuwapanga wafanyabiashara (machinga) katika maeneo maalum kwa lengo la kuwajengea mazingira (miundo mbinu) wezeshi ya kufanya biashara; Kutoa mafunzo maalum kwa wamachinga; Kuwepo na dawati maalum litakaloshughulikia Sera na Miongozo pamoja na kuboresha vitambulisho vya machinga.

Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya alieleza Washiriki kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweka miundombinu kwa maana ya jengo, imewapanga wamachinga na kuwapa vitambulisho. Alionesha kazi hii ya miundombinu kama “Hardware” na kwamba ili Mmachinga aweze kufanya biashara endelevu basi kunahitajika kuwepo kwa “Softaware”. Aliwaeleza washiriki kwamba MKURABITA imeonesha njia na ni mwanzo mzuri kwa wadau wote kutafakari namna bora ya kuandaa hiyo “Software” itakayowawezesha wamachinga kuifanya biashara ionayokua.

Awali, Mtendaji Mkuu wa MKURABITA, CPA. Dkt. Seraphia Mgembe alielezea lengo la kuendesha Kikao cha Wadau ni: kuandaa Mpango mkakati wa kuwawezesha Machinga kushiriki katika ujenzi waTaifa kwa kuwa wana fursa ya kujenga uchumi kupitia biashara zao. Dkt. Mgembe alieleza kuwa mpango uhusishe kuwajengea uwezo kwa njia ya mafunzo, sambamba na uwepo wa Kituo jumuishi cha urasimishaji na uendelezaji biashara, na uwezeshwaji wa mitaji kwa kuunganishwa na taasisi za fedha.

Taasisi zilizoshiriki katika mafunzo hayo ni: Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara,Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Jeshi la Polisi Jamii, Shirikisho la Umoja wa Machinga Mkoa wa Dodoma na Taasisi za Fedha (Mabenki).