Tanzania emblem

The United Republic of Tanzania

Property and Business Formalization Program

News

URASIMISHAJI BIASHARA ZA BODABODA/BAJAJI MBIONI KUANZA-MKURABITA


Kaimu Mkurugenzi wa Kurasimisha Ardhi na Biashara wa Mpango wa Kurasimisha Ardhi na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Jane Lyimo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wakati wa kuwasilisha Taarifa ya Tathmini ya Utafiti wa Msingi wa Biashara ya Bodaboda/Bajaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma leo Agosti 11,2021.

Akizungumza katika kikao hicho, Lyimo amesema kuwa lengo la utafiti huo ni kuandaa mpango wa kurasimisha shughuli za waendesha bodaboda na bajaji ili wawe kwenye mfumo rasmi wa kuaminiwa kukopesheka na taasisi za fedha kuboresha maisha yao kiuchumi.

Lyimo amesema kuwa shughuli za urasimishaji wa vyombo hivyo, unaakisi dhana ya mpango wa Mkurabita wenye lengo la kuwawezesha wananchi kurasimisha rasilimali na biashara wanaomiliki na kuzitumia kama nyenzo ya kujiongezea kipato, mitaji na kupanua wigo wa ushiriki katika uchumi wa kisasa, unaoongozwa na sheria na kanuni za uchumi wa soko la ushindani.

Aidha, Lyimo amesema kuwa utafiti huo ulifanyika jijini Dodoma ni maandalizi ya uzinduzi wa urasimishaji wa shughuli hizo kwa nchi nzima ambapo wataanzia Makao Makuu ya Nchi Dodoma.

Naye, Afisa Urasimishaji na Uendelezaji Biashara wa MKURABITA, Zabron Makoye ameeleza jinsi utafiti ulivyofanywa na matokeo yake kuwa walianza kwa kukusanya dodoso za waendesha bodaboda/bajaji zilikusanywa kwa kwa kutumia simu janja na kwamba dodoso hizo zilitumika kupata taarifa za biashara.

Amesema kuwa uchambuzi wake ulilenga kupata taarifa za mahitaji halisi ya biashara hiyo ili kuwezesha timu ya urasimishaji kupanga vizuri mafunzo yaliyolenga kutatua changamoto ambazo wafanyabiashara walengwa wanakumbana nazo.