Tanzania emblem

The United Republic of Tanzania

Property and Business Formalization Program

News

Mkuu wa Wilaya ya Bahi atoa pongezi kwa MKURABITA…


Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamis A. Mugunda ameipongeza MKURABITA kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuhuisha mitaji ya wananchi kwa kurasimisha ardhi na biashara zao ili kuwawezesha kiuchumi. Mkuu wa Wilaya alitoa pongezi hizo alipotembelewa na wawakilishi wa MKURABITA waliofika ofisini kwake kwa lengo la kutambulisha mradi wa urasimishaji ardhi vijijini unaotekelezwa katika vijiji vya Makanda na Msisi wilayani Bahi. Alieleza kwamba anatambua kuwa kuzifikia zaidi ya Halmashauri 60 kwa utaratibu wa kurasimisha ardhi za wanyoge sio kazi ndogo ikizingatiwa kwamba Tanzania ni kubwa na ina Halmashauri nyingi, hivyo mnastahili pongezi kwa kusaidia kutufungua macho tuone utajiri uliofichika katika mali za wanyonge.

Aidha, Mhe. Mwanahamis aliahidi yeye na ofisi yake kutoa ushirikiano kwa kufanya uhamasishaji kwa wananchi wa maeneo yanayotekeleza mradi huu pia maeneo ya vijiji vingine vilivyobaki ila nao wao waone umuhimu wa kujipanga kutekeleza urasimishaji katika maeneo yao. Aliongeza kwa kusema kwamba ujio wa mradi huu katika Halmashauri ya Bahi kutasaidia kupu guza migogoro ya ardhi isiyoya lazima hivyo kuwawezesha viongozi na wananchi kutumia muda wao katika kufuatilia masuala mengine ya maeneleo badala ya kushughulikia migogoro ya ardhi.

Kutokana na umuhimu na faida za mradi wa urasimishaji, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliahidi kufanya utaratbu wa kuandaa mafunzo elekezi kwa ajili ya waheshimiwa madiwani, wenyeviti wa vijiji watendaji ngazi ya kata na vijiji pamoja na maafisa tarafa ili wasaidie katika kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kuhusu faida za urasimishaji. Pia aliwataka watendaji wa Halmashauri kusimamia kwa karibu mipango kina ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa katika baadhi ya vijiji. Hii ni kwa sababu imeonekana katika baadhi ya vijiji vyenye mipango ya matumizi ya ardhi wananchi hawazingatii mipango hiyo pamoja na kuwepo kwa sheria ndogo za usimamizi wa matumizi sahihi ya ardhi katika vijiji vyao.

MKURABITA ambayo mpaka sasa imefanikiwa kujenga uwezo katika Halmashauri za wilaya 60 za Tanzania Bara na wilaya nne (4) za Tanzania Zanzibar inatarajia kukamilisha zoezi la urasimishaji ardhi katika vijiji viwili vya wilaya ya Bahi katika kipindi cha miezi miwili. Sambamba na urasimishaji ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999. Mashamba yapatayo 3,000 yanatarajiwa kurasimishwa sambamba na wamiliki wa mashamba hayo kujengewa uwezo kwa kutoa mafunzo ya namna ya kuungwanishwa na huduma za mitaji kupitia taasisi za fedha na kilimo bora. Pia MKURABITA itawezesha ujenzi wa ofisi za masjala za ardhi za vijiji vya Msisi na Makanda ikiwa ni matakwa ya sheria husika. Halmashauri zingine zinazotarajiwa kunufaika na mradi kama huu kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Newala na Masasi.