April 11, 2018 Uncategorized 0 comment

Aliyoyasema Mgeni Rasmi, Mratibu wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais IKULU, BI. Ened Munthali Wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo kwa Wadadisi wa Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi Hapa Nchini

Serikali  imeagiza Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na  Biashara  Tanzania (MKURABITA) ambao  uko Chini  ya ofisi ya Rais  Ikulu kwa kushirikiana  na Ofisi  ya Takwimu ya Tanzania Bara na Ofisi ya Mtwakwimu  Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, kufanya utafiti  wa sekta  isiyo rasmi  nchini kwa lengo la kubaini hali halisi  ya sekta hii kwa sasa.

Utafiti huu ni Wanne kufanyika nchini baada ya ule uliofanyika mwaka  1991ambao  ulibaini  kuwa asilimia  10.5 ya Wananchi  walikuwa  wanaendesha shughuli zao  Katika sekta isiyo rasmi. Utafiti  wa pili ulifanyika  mwaka 1995 na kuonyesha kuwa asilimia 9.5 ya      wananchi wanaendesha shughuli zao  katika mfumo usio rasmi. Utafiti wa tatu ulifanyika mwaka 2005 na kubainisha kuwa asilimia 89 ya Ardhi nchini haikuwa rasmi na asilimia 98 ya biashara ziliendeshwa katika  sekta  isiyo  rasmi.

Mwaka 2003/2004, Serikali ilifanya uamuzi wa kuanzisha MKURABITA kwa lengo la kurasimisha Ardhi na Biashara ili kupunguza ukubwa wa tatizo la sekta isiyo rasmi nchini. Serikali  imeamua kufanya utafiti ili kufathmini  na kubaini  ukubwa wa sekta isiyo rasmi nchini kwa ajili ya  mipango ya maendeleo. Matokeo ya utafiti wowote yanategemea usahihi wa taarifa  zinazokusanywa na wadadisi.

Taarifa za utafiti  huu zitakusanywa kwa mfumo wa TEHAMA. Taarifa za utafiti huu zitatumika kufanya tathmini ya mipango na program mbalimbali zilizotekelezwa  na Serikali  na wadau wengine katika uboreshaji  wa umiliki wa biashara  na rasilimali kwa wananchi  wanyonge nchini. Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara na Zanzibar zimejipanga vyema kuhakikisha kuwa Utafiti huu unakamilika kwa wakati  uliopangwa  na Kwa ubora. Wananchi wote wanao wajibu wa kutoa ushirikiano kwa wadadisi.

*IMEANDALIWA  NA IDARA YA HABARI – MAELEZO.