February 5, 2017 Uncategorized 0 comment

MKURABITA itabadilisha maisha ya wananchi wengi

MKURABITA kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Tume ya Mipango Zanzibar imeandika historia kwa kuwezesha kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Shehia Kiungoni katika wilaya ya Wete, Pemba. Jengo hilo lilifunguliwa rasmi na Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambaye alikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo la Ofisi ya Shehia Kiungoni. Hafla ya ufunguzi wa jengo hilo ilifanyika katika viwanja vya Ofisi ya Shehia Kiungoni tarehe 7 Januari 2017 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.

MKURABITA itabadilisha maisha ya wananchi wengi..”, haya yalisemwa na Mh. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa wakati wa ufunguzi wa jengo hilo akiwahutubia wananchi. Aliwapongeza kwa kuwa wapenda maendeleo na aliwasihi waendelee kuwa hivyo. Aliwaeleza kuwa kitendo cha kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi hiyo ni upendo mkubwa kwa kuwa wengine wangedai walipwe fidia. Alisisitiza kuwa jengo hilo ni la wananchi hivyo walipokee kwa ajili ya kuleta maendeleo yao.  Aliishukuru MKURABITA kwa kuwezesha urasimishaji katika Shehia mbalimbali huko Zanzibar ikiwemo Shehia ya Chokocho ingawa huko MKURABITA hawajajenga jengo kama hilo la Kiungoni.

Aidha, aliwaeleza wananchi kuwa MKURABITA ni Mpango mzuri kwa kuwa unaondoa migogoro ya ardhi, pia huinua mitaji ya wananchi na kuwaletea maendeleo. Pia alitoa hisia zake kuhusu matatizo ya migogoro ya ardhi, ambapo alikiri kuwa yeye ni mhanga wa kutapeliwa na kudhulumiwa ardhi yake huko Pemba. Hivyo, aliwaomba masheha kusimamia mauzo ya ardhi kwa umakini na kutunza kumbukumbu za mauzo hayo ipasavyo. Mh. Mbarawa alisema kuwa anaamini kwamba MKURABITA ujenzi wa aina ile katika maeneo mengine. Aliwahakikishia wananchi kuwa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania, utabadilisha maisha ya wananchi wengi hapa nchini kupitia urasimishaji.

Kuhusu hali ya kisiasa, hakusita kukemea tabia za baadhi ya viongozi wanaowagawa wananchi kwa misingi ya kiitikadi. Alisema kuw, kiongozi mzuri ni yule anayewaleta wananchi karibu na kuwaweka pamoja kwa ajili ya maendeleo yao. Mwisho aliiomba MKURABITA isiitupe mkono ofisi hiyo, bali ifuatilie na kutathmini matumizi yake kwa ufanisi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wananchi wengi pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini. Baadhi ya viongozi waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Khamis Athuman, Mkuu wa Wilaya ya Wete Mh. Rashid Kharid Rashid, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa MKURABITA Mh. John Z. Chiligati na baadhi ya wajumbe wa Kamati, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Ndg. Khamis Rashid Ali, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Dkt. Juma Hassan Reli na Bw. Omar Khamis Othman Sheha wa Shehia ya Kiungoni. Vikundi mbalimbali kikiwemo kikundi cha ngoma ya Uringe kutoka Micheweni kilitumbuiza pamoja utenzi na ngonjera iliyosomwa na vijana kutoka shule ya sekondari huko Wete.

Katika ujenzi wa jengo la Ofisi ya Shehia ya Kiungoni, MKURABITA imechangia kiasi cha TShs. 62,896,000.00 ambapo wananchi wa shehia hiyo wamechangia nguvu kazi na ardhi kwa ajili ya jengo hilo. Shughuli za ujenzi wa jengo hilo zilienda sambamaba na urasimishaji wa mashamba huko Kiungoni ambapo jumla ya viwanja 1,030 vimetambuliwa. Utekelezaji wa MKURABITA kwa upande wa Zanzibar uko chini ya uratibu wa Tume ya Mipango ambapo  viwanja 885 vimetambuliwa katika Shehia ya Chokocho na viwanja 1,600 vimetambuliwa katika eneo la Nungwi. Katika Shehia ya Welezo viwanja 2,500 vimepimwa na viwanja 1,100 vimetambuliwa katika Shehia ya Chwaka. Aidha, Vile vile, katika eneo la Chwaka viwanja 1,100 vimetambuliwa na viwanja 1,100 katika Shehia ya Limbani pamoja na viwanja 685 katika eneo la Jang’ombe.