August 30, 2016 Uncategorized 0 comment

Wabunge Waishauri Serikali Kuiwezesha MKURABITA Kibajeti

Hivi karibuni MKURABITA ilipata bahati ya kutembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambao walifika kwa lengo la kujifunza na kufahamu zaidi kuhusu madhumuni na utekelezaji wa shughuli za Mpango huu.

Kamati ilipokelewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mh. Angela Kairuki (Mb) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu Ikulu Bw. Peter Ilomo pamoja na Mratibu wa MKURABITA Bi. Seraphia Mgembe.
Wajumbe wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Pudenciana Kikwembe (Mb) walipata fursa ya kuelezwa juu ya changamoto zinazoikabili MKURABITA na jinsi inavyokabiliana nazo pamoja na mipango ya baadaye katika kufanikisha lengo la kuanzishwa kwa MKURABITA nchini.

Baadhi ya jitihada hizo ilielezwa kuwa ni pamoja na uanzishwa wa mfuko wa urasimishaji na umuhimu wa kuanzishwa kisheria kwa chombo mahsusi kitakacho ratibu shughuli za urasimishaji nchini.
Baada ya kupokea taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Mpango kuhusu MKURABITA, wajumbe kwa pamoja waliipongeza MKURABITA jinsi inavyotekeleza shughuli zake na jinsi inavyokabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti.

Aidha, wajumbe waliishauri Serikali kuongeza bajeti ili kuwezesha MKURABITA kutekeleza dhana ya uwezeshaji kwa ufanisi zaidi ili kuwafikia wananachi walio wengi. Kamati pia iliielekeza kwa MKURABITA kuwekeza katika utoaji elimu kwa umma kuhusu uwepo wa Mpango huu na jinsi inavyofanya kazi pamoja na manufaa yake kwa wananchi.
Walisisitiza kwamba kwa kuitangaza MKURABITA kutawawezesha wananchi wengi kushiriki katika shughuli za urasimishaji na kunufaika zaidi kiuchumi.

Aidha, wajumbe walielezwa kusikitishwa kwao kuhusu suala la baadhi ya taasisi za fedha kutozitambua Hati Miliki za Kimili ambao walishauri kuwa serikali itoe waraka maalum wa kuzitaka taasisi za fedha kuzitambua na kuzipokea hati hizo ambazo baadhi hutolewa kupitia urasimishaji ardhi unaofanywa na MKURABITA.
Wajumbe walienda mbali zaidi kwa kuonesha hofu yao kuwa neno wanyonge pengine linachangia kuwa ni kikwazo. Hivyo, walishauri Serikali kupitia MKURABITA itafute tafsiri nzuri zaidi itakayoonekana kuwatia moyo wananchi tofauti na ilivyo.

Waliendelea kwa kusema kwamba inavyoonekana kwa sasa ni kama kuendeleza fikra za mwananchi kujiona wanyonge tafsiri ambayo huenda inayochangia hata kwa Hati Miliki za Kimila kuonekana ni za kinyoge na kukataliwa katika baadhi ya mabenki.

Akihitimisha ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati Dkt. Kikwembe (Mb.) alieleza kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa dhana na shughuli za MKURABITA, kuna haja ya kuhakikisha mbinu mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vitumike katika kujitangaza na kutoa elimu kwa jamii ili wananchi wanufaike na Mpango huu.
Pia alishauri MKURABITA inapokwenda kutoa elimu, ihakikishe ina shirikisha na wadau pamoja na wawekezaji yakiwemo mabenki ambao ndio mkombozi wa wananchi.

Alitilia mkazo zaidi suala la kuwashirikisha na kuwawezesha wanawake na vijana kwa kuwapatia elimu ili wawe na ufahamu wa kutosha na sahihi kuhusu urasimishaji na umiliki wa ardhi kwani walio wengi hawamiliki ardhi kutokana na baadhi ya mila zilizopitwa na wakati katika jamii zetu.